RIWAYA YA MWANAFUNZI MCHAWI SEHEMU YA KUMI NA MBILI

Mwanafunzi Mchawi (A Wizard Student) - Sehemu ya Kumi na mbili
MTUNZI:ENEA FAIDY
....DORICE alimtazama malkia yule kwa woga huku fimbo ile ya dhahabu ikiwa kifuani mwake. Alihisi kifo chake kipo njiani lakini akajipa moyo wa imani kuwa hawezi kufa kwani hakutenda kosa lolote. Malkia Yule alicheka kicheko kikali cha kutisha.
"Dorice wewe in mchawi sio?" Alisema Malkia yule huku akiwa na sura ya kutisha sana.
"Mimi sio mchawi!" Alijibu Dorice kwa kutetemeka.
"Mbona ulipovamiwa na chatu pale njiani uliongea maneno ya kichawi?"
"Ndio niliyaongea lakini mimi so mchawi, maneno hayo nilifundishwa na babu yangu ambaye ni mganga!" Dorice alishikwa na woga kupita kiasi.
"Hahah Dorice... Kuwa mkweli?"
"Kweli kabisa.. Mimi si mchawi.. Tafadhali naomba mniruhusu niende!" Alisema Dorice huku akilia.
"Unaenda wapi?"
"Naenda Singida kwa babu yangu!"
Aliomba Dorice akiwa amepiga magoti huku akilia kwa hofu.
"Huwezi kwenda Dorice... Sahau kuhusu kuondoka hapa!" Alisema malkia yule kisha akamwamrisha mlinzi wake amwondoe pale Dorice ampeleke sehemu nyingine.
Mlinzi alitii agizo la malkia akamtoa Dorice pale na kumpeleka eneo lingine.
Kilikuwa kama chumba kidogo chenye mwanga hafifu lakini kilikuwa na mapambo mengi sana ya dhahabu. Kilipendeza sana na kilivutia macho kupita kiasi, Dorice alibaki anashangaa.Aliingizwa chumbani mle bila kuambiwa kitu chochote na mlango ukafungwa. Akabaki peke yake.
Hofu ilimzidia sana alitetemeka kama MTU aliyekumbwa na baridi Kali sana, hakupata fursa ya kutazama kitu chochote ndani ya chumba kile akabaki ameinama huku akilia. Alijuta kutoroka shule kwaajili ya Doreen, aliona heri angebaki tu kuliko kuchukuliwa na viumbe wale wa ajabu.
Ghafla akiwa katika dimbwi zito la mawazo alishtuliwa na sauti nzito ya kiume ikimwita jina lake."Dorice" Dorice alishtuka sana kwani alipoingizwa mle hakukuwa na mtu yeyote wala hakusikia mlango ukifunguliwa.Aliinua kichwa na kumtazama aliyemwita.
"Usiogope Dorice.. Naitwa Mansoor, ni mtoto wa Malkia.." Alijitambulisha mwanaume Huyo mwenye sura nzuri ajabu, alinukia marashi mazuri sana yasioisha hamu kuyanusa. Dorice alishangazwa na uzuri wa kiumbe yule mwenye umbo tofauti na viumbe wengine aliowaona kwenye eneo lile. Kwa haraka alimkadiria kuwa na umri wa miaka kama 21 au 22.
"Dorice! Nimeshangazwa sana na uzuri wako uliojaaliwa.. Ama kweli umeumbika! Karibu kwenye himaya yetu!" Alisema kijana yule aliyejitambulisha kwa jina la Mansoor huku akitabasamu na kumpa mkono Dorice. Dorice alibaki ameduwaa kwa mshangao.
****
Eddy alikuwa bado ana hali mbaya iliyomliza sana mama yake kwani Hakuwa na mtoto mwingine yeyote zaidi ya Eddy. Kila Mara alimtazama Mwanaye kisha akatikisa kichwa kwa majonzi. Kwa wakati huo baba yake Eddy alikuwa hayupo nyumbani, alikuwa yupo Dubai kwaajili ya buashara zake.
"Eddy mwanangu una nini?"
"Sina tatizo mama! Naomba nirudi shule..!" Alisema Eddy huku akilia.
"Huna tatizo wakati una tatizo kubwa? Eddy mwanangu nakufahamu vizuri, hebu niambie una tatizo gani?"
"Sina tatizo... Naomba chakula!"
"Nakupa ila naomba uniambie..!"
"Nitakuambia mama ila ngoja baba arudi!"
Mama Eddy hakuishiwa maswali kwa mwanaye, alitamani ajue anasumbuliwa na nini lakini jitihada zake ziligonga mwamba. Eddy hakuwa tayari kumweleza chochote.
Mama Eddy alimwandalia chakula akipendacho mwanaye. Wali na samaki aina ya Sato vilikuwa tayari vipo mezani vikimsubiri Eddy avishughulikie. Eddy alikitazama chakula kile kisha akaachia sonyo Kali.
"Mama! Hivyo ndio nini? Ntakulaje chakula kina harufu kama nini? Huoni hao funza walivyojaa humo au ndio chakula chenu siku hizi?"
Alisema Eddy akiwa amekunja sura kama amekula ndimu iliyooza.
"Funza? Funza wako wapi?" Mama Eddy alishangaa kwani chakula kile ndio kwanza alitoka kupika mda ule.
"Funza hao! Huoni wanavyotembea tembea humo kwenye bakuli? Mama toaaaa..!" Alisema Eddy kwa sauti.
"Mmh! Mwanangu we umerogwa.. Sio Bure..!" Alisema mama Eddy huku akiondoa chakula kile mezani.
"Eddy kweli umeona funza?"
"Ndio kwani we hujaziona?" Eddy Alisisitiza na kuzidi kumshangaza mama yake.
Mama Eddy alizidi kuchanganyikiwa, akachukua simu na kumtafuta baba yake Eddy.
"Hebu achana na hizo biashara baba Eddy! Mtoto ana hali mbaya sana!" Alisema mama Eddy kwa msisitizo.
"Kwani ananini?"
"We njoo mume wangu, uje haraka sana!"
"Mh! Leo nakata tiketi ya ndege nakuja!"
Mama Eddy alikata simu kwani alikuwa amempigia mumewe kupitia mtandao wa IMO.
Kesho yake baba Eddy aliwasili nchini na kufika nyumbani kwake haraka.
Alipomtazama Eddy hakuona kama ana tatizo sana. Aliona yupo kwaida na alishindwa kuelewa ni kwanini mkewe alichanganyikiwa kiasi cha kumfanya aache biashara zake na kurudi nyumbani.
"Wanawake bhana mbona Eddy mzima kabisa?"
"Mzima? Amerogwa huyu mume wangu tangu.. afike Jana hajala kitu anasema eti anaona funza?"
"Eti nini? Mbona sielewi? Hujazoea utani wa Eddy mke wangu!?" Baba Eddy alichukulia kimasihara suala la Eddy. Ikabidi wamkalishe chini na kumuuliza vizuri kilichomsibu kijana wao.
Sikh hiyo Eddy alikuwa mpole kupita kiasi, ni kama vile akili zilirudi kichwani mwake.
"Baba! Mama! Hapa nilipo sio MTU tena, siwezi kuishi tena kwani nikiishi sitakuwa mkamilifu.. Bora nife!"
Maneno hayo ya Eddy yalikuwa kama upanga kwani yalichoma mioyo ya wazazi wake na kuiachana katikati huku damu zikichuruzika bila kikomo.
"Eti nini Eddy!"
"Bora nife!" Aliridia Eddy
"Kwasababu gani? Tumekukosea nini? Kuna kitu hatujakupa?"baba Eddy alichanganyikiwa na kuinuka sofani kama amechomwa na mwiba.
"Wazazi wangu! Nimefanywa vibaya na binadamu katili, nimechukuliwa.. .. Ah.. Nime..!" Eddy aliangua kilio na kushindwa kuendelea kuongea.
"Sema tu.. Umechukuliwa pesa? Au umebiwa vitu vyote sema tu.." ****
"Doreen unataka nini kwangu?" Aliuliza Nadia Joseph.
"Sitaki kitu.. Nataka tupige stori..."
"Stori zipi za kutaka kuniwangia mchana kweupeee?"
Maneno ya Nadia yalimshtua sana Doreen, hakutaka kuamini kama Nadia amejua lengo lake alistaajabu kidogo lakini hakutaka kushindwa.
"Doreen unataka kuniwangia? Usitake kunijaribu nitakuaibisha!" Alisema Nadia kwa sauti ndogo iliyosikika vizuri.
Doreen bado hakumuamini akajiweka sawa, akataka atumie ufundi na nguvu za uchawi wake ili amtulize kimya Nadia. Akaachia kombora lake la kichawi lakini....
Itaendelea....

Related Post

Previous
Next Post »