RIWAYA:MWANAFUNZI MCHAWI
MTUNZI:ENEA FAIDY
Sehemu ya 40
....Eddy alisimama kwa muda huku akiyashangaa yote yanayoendelea. Alishindwa kuamini kama kinachoendelea pale kilikuwa na ukweli ndani yake. Alifuta macho yake na kutazama tena, safari hii macho yake yalitua moja kwa moja kwa Doreen aliyekuwa amepiga magoti mbele yake huku akilia kwa uchungu na majuto mengi.
"Nisamehe Eddy kwq kukufanyia ukatili huu. Nimekutesa sana wewe na familia yako... Nisamehe tafadhali" alisema Doreen huku akilia kwa uchungu hali iliyodhihirisha majuto aliyokuwa nayo moyoni mwake. Hata hivyo Eddy hakuweza kuzungumza chochote zaidi ya kumtazama Doreen kwa hasira huku machozi yakimtiririka machoni mwake. Aliumanisha meno yake kwa hasira huku akitamani kuiondoa roho ya Doreen kwani mateso aliyompa maishani mwake ilikuwa ni vigumu kusahaulika. Mateso aliyokuwa nayo yalijaa fedheha na aibu isiyositirika. Machozi yalimshuka taratibu machoni mwake huku akimtazama Doreen.
"Naomba unisamehe Eddy ili adhabu ninayopata ipungue walau kidogo... Nateseka Eddy" Doreen alizidi kumsihi Eddy lakini maneno yake ilikuwa ni kama kujilisha upepo kwani Eddy hakuukubali msamaha wake.
Wanawake waliokuwepo eneo lile walijisikia aibu kwa kuona wanawake wenzao wapo uchi wa mnyama. Wakatoa khanga zao na kuwapa akina Doreen wazivae lakini hata hivyo ilikuwa vigumu kwa akina Doreen kupokea khanga zile kwani maumivu yalikuwa Makali mno kwenye miili yao. Kila Mara walihisi moto ukiwawakia katika ngozi zao. Ikawabidi wanawake wale wawafunike kwa lazima ili kuwasitiri.
Ghafla mwili wa Maimuna ukaanza kubadilika na kuwa mweusi kama mkaa. Akajiviringa viringa kama nyoka pale sakafuni huku akitoa mlio kama wa mbuzi kisha akatoweka mbele ya macho ya watu. Wote waliogopa sana, baadhi ya watu walijikaza kisabuni na kuendelea kubaki pale huku wengine wakikimbia sana na kuondoka eneo lile.
Doreen alibaki pale huku akiendelea kumsihi Eddy amsamehe. Lakini Eddy alikuwa na moyo mgumu sana wa kumsamehe kiumbe yule.
"Hustahili kuishi Doreen... Kufa tu.." Alisikika Eddy kwa sauti iliyojaa hasira.
"Kweli! Afe tu huyu! Tumuue!" Walisikika Raia waliokuwepo eneo lile.
"Nitakufa ndio ila naomba unisamehe.. Najua nimekukosea sana... Sitaki nife kabla hujanisamehe!" Alisema Doreen.
"Kwa mateso uliyonipa siwezi kukusamehe... Umenitesa sana... Sijui nani amekuadabisha namna hii na kukudhalilisha hivi... Amenifurahisha sana" alisema Eddy kwani hakujua lolote linaloendelea kuwa Dorice ndiye aliyefanya yote hayo.
"Na kwa jinsi ulivyonifanyia.. Daima siwezi kumwamini mwanamke! Naapa!" Alisema Eddy lakini kuna sauti ilimnong'oneza masikioni mwake
"Usiseme hivyo... Niamini Mimi" Eddy alishtuka sana akaangaza macho huku na kule pasipo kuona mtu aliyemnong'oneza. Sauti ile haikuwa ngeni sana masikioni mwake ila alishindwa kujua ilikuwa ya nani. Akatafakari kwa muda kisha akaipotezea sauti ile na kuendelea kumtazama Doreen.
"Eddy hutaki kunisamehe?" Aliuliza Doreen kwa sauti ya upole. Eddy akatafakari kidogo, akagundua kutomsamehe binadamu mwenzake ni kosa kubwa kwani yeye hutenda dhambi nyingi lakini husamehewa na Mungu.
"Nimekusamehe.. Ila sitokusahau!"
"Asante..."
Wakati akizungumza hivyo ghafla haja ndogo ilimbana sana Eddy, hakuielewa hali ile kwani tangu sehemu zake za siri ziondolewe hakuwahi kubanwa na haja ndogo hata Mara moja. Eddy alijishangaa sana akaamua kukimbia na kwenda msalani ili kuona kama angeweza kutoa taka mwili inayojulijana kama mkojo.
Alipofika chooni alishusha kidogo suruali yake na bila kutarajia akakuta sehemu zake zimerudi. Eddy hakuamini macho yake, akataka kujihakikishia kama kweli zitafanya kazi. Akakojoa na kweli jaribio lake likazaa matunda kwani alifanikiwa kukojoa kwa Mara ya kwanza.
"Mungu wangu! Mbona siamini!" Alisema Eddy kwa mshangao na furaha ya ajabu. Akajikuta anaruka ruka kule chooni shangwe kuu. Ghafla akahisi kuna mtu nyuma yake, Eddy akageuka haraka na bila kutarajia akakutana na uso uliojaa tabasamu wa Dorice.
"Eddy mpenzi nakupenda sana.. Nimefanya yote Haya kwaajili yako... Ili uone thamani ya upendo wangu.. Narudia tena niamini Mimi! Nakupenda!" Alisema Dorice. Eddy alibaki kimya akiwa ametoa macho kwa mshangao.
"Wewe ni jini"
"Hapana!"
"Sasa umefikaje hapa"
"Sina nia mbaya.. Nilitaka tu nikusaidie kwa tatizo lako... " alisema Dorice.
"Asante sana... Nashukuru Dorice... " alisema Eddy na kumkumbatia Dorice bila woga.
"Unanipenda?"aliuliza Dorice.
"Nakupenda sana!" Alisema Eddy kisha wakakutanisha midomo yao na kupeana mabusu. Licha ya kwamba Dorice alifahamu fika kuwa kufanya vile lilikuwa kosa kubwa sana kwa Mansoor lakini hakujali hilo kwani upendo wake wote ulikuwa kwa Eddy, alimpenda kupita kiasi.
"Wewe ndo mwanaume wa maisha yangu Eddy... Tangu nimekutana nawewe siku ya kwanza na ukanambia unanipenda sikutamani uniache hata kwa sekunde moja" alisema Dorice kwa sauti iliyojaa huba.
"Nakupenda pia Dorice... Wewe ni mwanamke pekee uliye kwenye ndoto zangu" alisema Eddy.
"Asante Eddy nitakuja wakati mwingine" alisema Dorice na kupotea.
"Doriiiiiice! Usiache kuja" alisema Eddy kwa sauti lakini Dorice alikuwa ameshaondoka.
Eddy alitoka nje akiwa na furaha sana. Alitamani hata kumwonesha kila mtu sehemu zake za siri ili ajue kuwa anazo.
Alipofika pale nje alikuta Doreen anavuja damu sana kwani wananchi walishaanza kumtupia mawe. Polisi walikuwa wamefika tayari eneo lile na kumchukua Doreen ili asiumizwe zaidi. Kwa mbali alionekana Dorice akimtazama Doreen na kumwambia kuwa yeye ndiye aliyefanya yote Yale. Lakini alipokuwa akizungumza hakuna aliyemwona zaidi ya Doreen na Eddy.
Doreen alichukuliwa na gari ya polisi na kupelekwa hospitali ili akatibiwe majeraha yake.
Lakini hata hivyo watu wengi walifika mpaka hospitali ingawa hawakuruhusiwa kuingia.
Doreen alianza kusaidiwa na madaktari , na baada ya kufungwa majeraha yake aliwaomba kitu madaktari.
"Kabla sijafa naomba mniitie mchungaji pamoja na waandishi wa habari" alisema Doreen kwa sauti ndogo iliyosikika kwa shida.
"Bado haupo vizuri... Unatakiwa kupumzika..." Alisema daktari mmoja.
"Tafadhali dokta nitajitahidi tu... Lakini cha kwanza nataka nikutane na hawa watu kabla sijafa..." Alisisitiza Doreen.
"Unataka kuwambia nini?"
"Kwanza nataka nitubu.. Pili Nataka niwaambie watu siri nzito kuhusu maisha yangu" alisema Doreen na kuwafanya madaktari wale washawishike na kufanya kama walivyoambiwa.
Alitwa mchungaji wa kanisa Fulani kisha wakaitwa waandishi wa habari wa vituo vya televisheni pamoja na radio ili warekodi kile alichotaka kuzungumza Doreen. Wote walikuwa na hamu ya kusikia kile wanachotaka kuambiwa na Doreen.
Na wakati huohuo taarifa za kilichomtokea Doreen zilikuwa tayari zimesambaa nchi nzima kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
MWISHO.
KAA TAYARI KWA MSIMU WA PILI WA RIWAYA HII UTAKAO KUJIA HIVI KARIBUNI. UTAPATA KUJUA MENGI YALIYOKUWA YAMEJIFICHA NYUMA YA PAZIA, UTABURUDIKA NA KUELIMIKA PIA.
JE UMEPATA FUNZO GANI??
1 comments:
Write commentsaisee uchawi upo...na dunian kuna watu na viatu tena chakavu visivyofaa kuvaliwa hata na wagonjwa wa akili....hadithi nzur...big up sanaaa
Reply