Mtunzi: Enea Faidy
==> Kama hukuisoma sehemu ya 16 <<BOFYA HAPA >>
..... MANSOOR alimtazama Dorice kwa jicho la kiulizo lililomtaka azungumze chochote lakini Dorice hakusema neno zaidi ya kuangua kilio cha huzuni baada ya kukosa msaada kwa Mansoor. Dorice alilia sana kwani alijua kurudi tena duniani sasa ni ndoto.
"Mansoor naomba unisaidie!" Dorice alipiga magoti akamsihi Mansoor aweze kumsaidia ili arudi kwao pia amsaidie kumwokoa Eddy ili furaha ya penzi lake irudi.
"Dorice! Naweza kukusaidia kwa yote hayo... Ila inabidi ukubali kuolewa na Mimi maana bila hivyo mama yangu hatonielewa...!" Mansoor alisisitiza.
"Siwezi kuolewa na wewe..!"
"Kwanini? Au kwa vile Mimi sio binadamu mwenzio? Jua nakupenda na nitakuruhusu kuendelea na Eddy.. Nielewe Dorice!" Mansoor alizidi kumweka Dorice katika wakati mgumu sana k wani kiukweli Dorice aliuhitaji msaada wa Mansoor ila masharti yake yalikuwa kikwazo sana. Dorice alishindwa kung'amua juu ya mtihani ule mzito.
Alijua fika wazazi wake wataumia sana endapo wakijua kuwa Hayupo duniani, aliyafikiria maumivu ambayo mama yake angeyapata kama yeye angepotelea kule kwenye ulimwengu wa majini.
"Sijui nimkubali halafu akinirudisha duniani nimkatae?" Dorice Alizidi kuwa na utitiri wa mawazo kichwani mwake. Ghafla akashtushwa na sauti nzuri ya mahaba ya Mansoor akizidi kumshawishi kuwa amkubalie ili aweze kumsaidia kutatua matatizo yake.
"Dorice! Nifanye nifurahi tafadhali.. Nilipendwa na wengi ambao si chaguo langu.. Nasikitika chaguo langu linakuwa mwiba moyoni mwangu! Kwanini lakini?"
Dorice alivuta pumzi ndefu na kuishusha taratibu, huku akiwa ameinamisha kichwa chake. Taratibu akanyanyua kichwa chake na kumtazama Mansoor. Macho yake yalistaajabu uzuri wa asili aliokuwa nao kijana yule. Hata kama majini ni wazuri lakini Mansoor alizidi kipimo, kuanzia macho yake, pua yake na midomo mizuri ya kupendeza sana.
"Nimekubali Mansoor! Ila kabla ya yote naomba uniahidi kama utanisaidia!" Alisema Dorice kwa sauti iliyotulia sana. Maneno hayo yalifungua ukurasa mpya moyoni kwa Mansoor, alifurahi kupita kiasi akamkumbatia kwa nguvu Dorice.
"Nakuahidi kukusaidia Dorice!" Alisema Mansoor akiwa amemkumbatia Dorice.
Walikumbatiana kwa muda kisha wakaachiana. Mansoor akamtazama Dorice huku akitabasamu.
"Nataka uvae vizuri nikupeleke kwa mama yangu muda huu!"
"Nitavaa nini? Sina nguo!"
Alisema Dorice kwa woga huku moyo wake ukimsuta kwa kumsaliti Eddy kwani alikwisha muahidi kuwa hatokuwa na mwanaume mwingine yeyote zaidi yake."lakini ni kwa sababu yake..!" Alijipa Jibu Dorice.
"Unapenda nguo gani?" Aliuliza Mansoor.
"Nguo yoyote itakayonifaa!" Alijibu Dorice.
Mansoor alinyoosha mkono juu ghafla ukatokea mfuko mmoja wenye ukubwa kiasi kisha akamkabidhi Dorice. Dorice aliogopa sana, akasita kupokea.
"Usiogope.. Chukua!"Dorice akapokea mfuko ule japo kwa woga kisha akaufungua ili atazame kilichomo. Akapigwa na bumbuwazi.
*****
Eddy aliwaacha wazazi wake barabarani pale wakiwa hawaelewi la kufanya. Walibaki wanatazamana kwa muda wa dakika tano nzima bila kusema neno lolote. Kila mmoja alionekana kutoelewa kilichotokea.
"Mr. Alloyce.. Tutakuwa wazembe tena wajinga... Mtoto ameondoka tumesimama tu kama milingoti hapa!" Alisema mama Eddy.
"Tufanyeje mke wangu?"
"Tumfuate!"
"Tutamfuata wapi sasa?"
"Kokote, kwani we hujaona alikokimbilia?"
"Dah! Tuna mtihani mzito!"
Ilibidi waingie msituni na kuanza kumsaka Eddy. Walimtafuta kila kichaka lakini hawakuona hata dalili za uwepo wa kijana wao. Jua liliwawakia huku wakizidi kumtafuta Eddy lakini bado hawakuona hata dalili za kumpata.
"Hili tatizo la kimwendokasi dah!" Alisema baba Eddy.
"Inabidi tulitatue kimwendokasi!"alijibu mama Eddy akiwa ameshika mkono kiunoni. Anahema kupita kiasi kutokana na uchovu aliokuwa nao.
"Mke wangu!"
"Abee.."
"Mimi naona turudi tu nyumbani hapa tutafanya kazi bure!" Alishauri Mr.Alloyce
"Nilishasema wewe humpendi mwanangu.. Turudi nyumbani halafu?"
Mama Eddy alimjia juu mumewe, akaona kama hana mapenzi wala uchungu kwa mwanae lakini baba Eddy alikuwa sahihi kabisa kwani mpaka pale walipofikia wasingeweza kumpata Eddy. Walikuwa wamechoka sana, pia wasingeweza kusonga mbele zaidi kutokana na ukubwa wa msitu waliokuwamo.
"Sikiliza mke wangu.. Nataka turudi tutafute njia sahihi ya kumtafuta mtoto hapa tunazidi kupoteza muda!" Kwa shingo upande mama Eddy aliamua kusikiliza ushauri wa mumewe.
Wakatembea umbali mrefu sana mpaka walipolifikia gari lao. Walipofika kwenye ile gari, kengele ya hatari iligonga mioyoni mwao wakatazamana kwa mshangao lakini hawakuwa na la kufanya kwani gari yao ilikuwa ikiteketea kwa moto mkali utadhani imemwagiwa petroli.
"Nini hiki?" Walijiuliza kwa pamoja bila kupata jibu la haraka. Ilibidi wasogee kwa ukaribu ili wahakikishe wakionacho. Ni kweli gari yao ilikuwa ikiwaka moto, na
ilikuwa hatua za mwisho kiasi kwamba hata wangezima moto ule bado gari yao isingesalimika.
"Haya maajabu!"
"Tena maajabu haswaaa ya ulimwengu..!"
Wakiwa bado wanaendelea kushangaa ajali ile ya moto kwenye gari ile, ghafla moto ukazima kama vile umezimwa kwa maji halafu gari ikatoweka machoni mwao.
Waliogopa kupita kiasi wakajikuta wanatimua mbio bila kutazamana.
Walikimbia sana wakiifuata barabara, kwa bahati mbaya mama Eddy alijikwaa na kuanguka chini kama gunia. Damu nyingi zikaanza kumtoka mguuni. Akapiga kelele Kali za maumivu, zilizokatisha mbio za Mr.Alloyce, akageuka nyuma na kumwona mkewe akivuja damu nyingi sana. Akarudi haraka.
"Vipi mke wangu?"
"Nime..nimeumia Mme..wangu..!" Mama Eddy aliongea kwa shida sana kwani alipata maumivu makali sana.
Walikuwa hawana hata mia mbovu mifukoni mwao kwani pesa zote waliziacha kwenye gari ambalo limepotea kimaajabu.
"Mke wangu" aliita baba Eddy baada ya kuona mkewe anakoroma isivyokawaida.
"Mama Eddy..!!!!!!"
*****
Mwalimu John alikuwa bado anatokwa na funza mguuni, alitaka kuieleza familia yake juu ya kile kilichompata lakini pindi alipotaka kuiambia familia yake juu ya mkasa ule mzito ghafla akapigwa kofi zito lililomrusha kama shoti ya umeme kutoka juu ya kiti mpaka chini. Alipiga yowe kali lililowashangaza watu wote sebuleni pale. Waliogopa sana.
Leyla mke wa Mwalimu John alimsogelea mumewe na kumwangalia kama yupo salama ghafla akapigwa na mshangao ulioambatana na furaha kwani miguu ya mwalimu John ilirudi katika hali ya kawaida na haikuwa na funza tena.
"Mume wangu!" Aliita Leyla kwa furaha, lakini John aliendelea kulalamika pale chini kwani Kofi alilopigwa lilikuwa zito kuzidi uzito wa mwili wake lakini hakujua limetoka wapi.
"Jamani.. Njoo muone maajabu..!"
Alisema Leyla akiwaambia ndugu wengine wa mumewe.Wote walimsogelea na kushangaa kilichotokea, wakakiri kwamba kweli dunia ina maajabu tena yanayotisha na kuogopesha.
Mwalimu John aligalagala pale chini kwa muda wa kama robo saa kisha taratibu akainuka. Alipotazama miguu yake aliifurahia sana kwani ilikuwa imerudi kwenye hali yake ya kawaida. Akainuka pale chini na kumkumbatia kwa furaha. Lakini cha ajabu kila alipotaka kuzungumza chochote..
*****
Doreen alibaki ametulia kimya pindi mlango unagongwa. Aliona anachofanya ni ujinga ni heri ainuke avae nguo kabla hajafumwa. Alipoinuka tu mlango ulifunguliwa. Doreen alishtuka sana kwani alikuwa yupo uchi wa mnyama na alikuwa amevaa shanga huku usoni amejipaka maungaunga na kumfanya awe na mwonekano wa kutisha.
Madamu Amina akiwa ameambatana na nesi wa shule walishtuka sana kumkuta Doreen akiwa vile. Walitazamana kwa mshangao kisha wakamtazama Doreen kwa hofu.
"Doreen unafanya nini?" Aliuliza Madam Amina kwa woga ingawa alijikaza tu. Doreen alibaki kimya tu bila kujibu chochote. Macho ya Madam Amina yalitua moja kwa moja kwenye kile kichupa cha dawa kilichokuwa pale chini tena kilikuwa kimefungwa kijitambaa kidogo cha kaniki kwa juu. Kiliwatisha sana.
"Doreen! Unafanya nini? Mbona hujibu?" Alisema nesi kwani walikuwa wamefikishiwa taarifa kuwa Doreen ni mgonjwa ndio maana amebaki bwenini.
Itaendelea.....
Usikose kufuatilia