RIWAYA YA MWANAFUNZI MCHAWI SEHEMU YA KUMI NA TATU

Mwanafunzi Mchawi (A Wizard Student) - Sehemu ya 13
 Mtunzi: Enea Faidy
 ===> Kama Hukuisoma sehemu ya 12 << BOFYA HAPA >>
....EDDY hakuwa na jinsi kwani aliona hana sababu yoyote ya kuwaficha wazazi wake juu ya tatizo lake.Aliamua kuwaambia ukweli Ili kama kuna uwezekano wa kumsaidia basi wamsaidie. Kwa kilio cha kwikwi kilichoonesha huzuni kuu iliyotawala moyo wake, Eddy alifungua kinywa na kusema ukweli.
"Sehemu zangu za siri... Zimepotea.. Sielewi zilikoenda!" Maneno ya Eddy yaliibua sura mpya kwa wazazi wake. Walishtuka mshtuko ambao haukuwahi kuwatokea maishani. "Ati nini? Hebu rudia tena..!" Mr.Alloyce hakuamini maneno ya mwanaye. Mama yake Eddy hakueweza hata kufumbua kinywa chake kwani alikuwa amechanganyikiwa kupita maelezo.
"Ndio hivyo baba yangu.. Sina raha ya kuwa hai..!" Eddy alizidi k ulia pindi alipozungumza maneno hayo.
Kiukweli kisa kile kiliwakata maini wazazi wa Eddy. Walihisi kuishiwa nguvu kabisa mwilini, walibaki kimya wakiwa wameinamisha vichwa vyao. Huzuni iliyochanganyika na mshangao ndiyo iliyotawala katika jumba lile la kifahari la Mr.Alloyce. Zilipita dakika tano kukiwa na ukimya wa kuogofya. Hatimaye Mr.Alloyce alivunja ukimya ule kwa kumdadisi mwanaye kwa maswali.
"Kuna mtu ulimkosea?"
"Hapana baba!" Alijibu Eddy.
"Sasa ilikuwaje mwanangu?" Mr.Alloyce aliuliza kwa sauti ya upole sana.
"Sijamkosea mtu ila kuna binti anaitwa Doreen..!" Eddy alitaka kusimulia jinsi ilivyokuwa lakini baada tu ya kutaja jina la Doreen hakuweza kuendelea kuzungumza kwani alipigwa Kofi moja zito, likamyumnisha pale kitini, kichwa kikamzunguka akahisi kama radi imempiga. Alipiga ukelele uliowashtua wazazi wake na kufanya wahamaki.
"Eddy nini?"Mr.Alloyce aliuliza kwa mshangao kwani alimuona Mwanaye akidondoka kitini bila kujua kinachoendelea.
Wakazidi kuchanganyikiwa sana, wakamsogelea Eddy na kumwinua lakini Eddy hakuwa na habari, alikuwa kama mzoga ambao unapelekwapelekwa kokote bila kutoa ushirikiano. Hali hiyo ilimtisha sana mama Eddy, akashindwa kuvumilia akaangua kilio kikali.
*******
Dorice aliendelea kumshangaa Mansoor bila kutia neno lolote, ingawa moyoni alibaki kumsifia kwa uzuri alionao mwanakaka yule bila shaka hakuna mwanamke ambaye kwa hali ya kawaida asingevutiwa nae. Yote hayo yalibaki moyoni mwa Dorice na asingeweza kusema lolote kwa kijana yule.
"Dorice mbona upo kimya wala hutaki kunijibu lolote.. Hata salamu?" Alisema Mansoor huku akiachia tabasamu mwanana.
"Mh! Umesemaje?" Dorice akajifanya hakusikia lolote.
"Ina maana hukunisikia kabisa..?"
"Ndio"
"Inawezekana kweli.. Maana unaonekana una mawazo mengi.. Unawaza nini?" Mansoor alimsogelea kwa ukaribu zaidi Dorice na kuketi.
"Nataka kurudi nyumbani!"
"Unataka kurudi? Kwasababu gani?"
"Siwezi kukaa huku! Nataka nirudi nyumbani!" Alisema Dorice huku machozi yakimlengalenga.
"Dorice! Utarudi vipi wakati mama yangu ameniambia amenitafutia mke? Nataraji kufunga ndoa nawewe hivi karibuni.." Maneno hayo ya Mansoor yalimshtua Sana Dorice akatoa macho kwa mshangao.
"Unasemaje wewe?" Dorice aliuvua woga akajikuta ameropoka kwa hasira.
"Sikiliza Dorice.. Kwa muda mrefu sana nilikuwa natafuta mke, sikumpata. Nilitamani sana kuoa binadamu ili niishi nae, na kwakuwa mama yangu ananipenda amenitafutia wewe na ninakupenda. Nataka nikuoe..!"
"Toka hapa.. Usinisogelee... " Alifoka Dorice na kumsukuma Mansoor.
Mansoor alihuzunika sana kwa kitendo alichofanyiwa na Dorice, akatikisa kichwa na kupiga hatua za taratibu kisha akatoweka ghafla machoni kwa Dorice. Dorice alishtuka sana akabaki ametumbua macho tu.
"Mungu wangu nisaidie niondoke huku, mkosi gani huu? Nitafanywa vibaya na viumbe hawa sijui majini... Bila shaka ni majini! Niolewe na jini? Siwezi Mimi...!" Alizidi kuwaza Dorice huku kijasho chembamba kikimtoka kwa kasi.
Ghafla mlango wa chumba alichokuwamo Dorice ukafunguka ghafla, Dorice alishtuka sana kukutana na sura ya malkia akiwa na hasira kupita maelezo.
"Dorice binadamu! Ungekuwa umeuwawa masaa mengi yaliyopita.. Lakini kutokana na mapenzi ya mwanangu Mansoor kwako ndio maana upo hai mpaka sasa.. Ni kitu gani kinakupa jeuri ya kumtesa mwanangu wa pekee?" Malkia alizungumza kwa sauti Kali iliyoambatana na radi. Alionekana mwenye hasira sana.
Dorice aliogopa sana wala hakuthubutu hata kunyanyua kinywa chake akabaki kimya huku akitetemeka.
"Dorice! Una machaguo mawili tu! Chagua moja... KUOLEWA NA MANSOOR AU KIFO!"
Alisema malkia yule kwa ukali, Hofu ikamzidia Dorice.
********
Doreen alipoathubutu kutumia uchawi wake kumdhuru Nadia Joseph, ghafla akakumbana na kichomi kikali sana ubavuni mwake. Akahisi maumivu makali yaliyomfanya apige kelele sana zilizowashtua darasa zima. Wanafunzi wote wakamgeukia yeye lakini kwa kukwepa aibu akajifanya kujinyoosha akiwa bado anaugulia maumivu
yale makali. Baada ya hapo wanafunzi wale wakaendelea na shughuli zao.
"Doreen.. Nakupa onyo, acha kuwachezea wenzio! Unajivunia uchawi lakini Mimi nina MUNGU.. Hunitishi kwa lolote maana niliyenaye ni mkuu kuliko nguvu zote.. Nimemwomba Mungu anioneshe MTU anayevuruga shule nashukuru sasa amenionesha! Achana na Uchawi!" Alisema Nadia kwa ujasiri sana ingawa aliongea kwa sauti ndogo ili asisikike sana.
Doreen aliumbuka sana, akaondoka bila kuaga.
Kengele iligongwa wanafunzi wote walitakiwa waende mstarini. Baada ya mkusanyiko wa wanafunzi wote alisimama mwalimu mmoja kwaajili ya matangazo muhimu.
"Kuuna taarifa za kusikitisha sana! Kiufupi ni kwamba Mwalimu Mkuu msaidizi na mwalimu wa taaluma hatuko nao tena. Wameaga dunia Leo asubuhi.. Pia kuhusu mwalimu John kuna sintofamu imetokea kiufupi ni kwamba hajafa bado yuko hai..." Wanafunzi walisikitishwa sana na taarifa zile ila walipigwa butwaa kuhusu mwalimu John kwani walikwisha tangaziwa kuwa amefariki lakini iweje waambiwe yuko hai? Walishindwa kuelewa.
Baada ya mwalimu kutoa matangazo aliondoka zake pale mstarini. Ndipo Nadia Joseph alipoomba nafasi ya kuzungumza na akapewa.
"Jamani wanafunzi wenzangu, hali hapa shule ni mbaya sana... Acheni masikhara hebu fanyeni maombi ya kweli! Mkisali kwa uaminifu MUNGU atajibu tu... Msichukulie mazoea tafadhali..." Aliposema hivyo kuna wanafunzi waliguna lakini Nadia hakujali hilo akaendelea.
"Sasa hivi wanataka titi la msichana.. Usipokua makini unaweza ukachukuliwa lako..!" Nadia aliposema hivyo, alimwona Doreen kwa mbali akiwa amenuna sana huku akimtazama Nadia utadhani anataka kummeza.
Wanafunzi wote wakataharuki, walianza kuogopa sana.
Nadia akaondoka pale mbele kisha wanafunzi wote wakatawanyishwa.
Doreen alikuwa na hasira za kuua MTU. Alimchukia Nadia kupita kawaida, akaahidi kumfanyia kitu kibaya sana....
Itaendelea....

Related Post

Previous
Next Post »