RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 35
Mtunzi:Enea Faidy
......OOH siamini! Siamini kabisa kama sioni nyeti za Eddy" alisema Doreen akiwa amechanganyikiwa sana. Alitazama vizuri kwenye mkoba wake lakini hakuona nyeti za Eddy na hakujua nani amechukua. Kutokana na ulinzi mkali aliokuwa ameuweka ili kulinda vitu vile hakutaka kuamini kama Kweli vimeibiwa.
Doreen alikaa kitandani huku akifikiria kwa muda ndani ya chumba kile cha hoteli. Mawazo yake kila yalipofurika kichwani mwake,jasho jembamba lilimtiririka kwa kasi. "Mbona sielewi hii hali?" Alijiwazia huku akijaribu kutafuta tena nyeti zile ambazo kwake zilikuwa na thamani kubwa kuliko lulu. Doreen alikaa chini kwenye sakafu huku mawazo yakizidi kumuelemea.
Akavua nguo zote kisha akachukua mkoba wake na kuchukua kioo kidogo, akakipaka dawa ya ungaunga kisha akaanza kuomba dua kwa mizimu yake ili iweze kumsaidia katika janga lile gumu lililomkumba. "Mzimu wa Ngotongoto uliomkubwa sana katika ukoo wetu, Mtukufu Tatile na mizimu yako...
Tazama nilivyohangaika na kutafuta zawadi kubwa kama nilivyoagizwa lakini Leo hii sijui ni mzimu gani uliotokea na kutaka kunyang'anya kitu cha thamani kuliko dhahabu... Kafara iliyonzuri kwa mkuu wangu... Nihurumieni mja wenu! Naomba msaada wenu tafadhali.." Doreen alisema maneno Yale kwa hisia Kali huku akiwa ameinamisha kichwa chake chini na mikono yake ikiwa imeshikilia kioo kile. " Ee mizimu yangu tukufu... Nisaidie kumjua mwizi wangu ili nimshughulikie..."
Alisema Doreen na ghafla radi Kali ikapiga kwenye kioo kisha kioo chote kikatapakaa damu. Doreen alishtuka sana akaona hali si shwari maana kioo kile kutapakaa damu kilikuwa na maana ya uwepo wa vita Kali dhidi yake. Hofu ikamtawala sana binti yule, hofu ikamtanda akashindwa kuelewa ni nani adui yake haswaa!. "Doreen! Doreen! Inakubidi kupambana!" Ilisikika sauti nzito yenye mwangwi mkali lakini mzungumzaji hakuonekana. "Doreen! Tumia nguvu zako zote ulizonazo, sisi tuko nyuma yako...
Onesha uwezo wako ili uutwae utukufu.. Uwe malkia uliyetukukaaa!!" Iliisisitiza sauti ile iliyoongea kwa msisitizo wa hali ya juu. Doreen aliogopa sana, akajua tayari mwisho wake umewadia lakini hakuwa na budi kujipa moyo wa ushindi na kuwa na matumaini ya kumbaini mbaya wake. "Nani mpinzani wanguuuu? Nasema nani atampinga Doreen Mbwana mtoto wa kitanga? Kama yupo ajeee!" Alisema Doreen kwa ujasiri wa hali ya juu na kuivua hofu yote aliyokuwa nayo.
Ghafla upepo mkali ukavuma kwa nguvu ndani ya chumba kile cha hoteli. Sauti Kali ya kicheko kilichojaa dharau na jeuri ikasikika na kumfanya Doreen ahamaki sana. Hali ya taharuki ikazuka moyoni mwa Doreen kwani daima hakufikiria kutokewa na mpinzani wa kumpinga mambo yake. "Doreen! Wakati wako umekwisha! Uchawi wako na mateso yako kwa wanadamu wasio na hatia sasa umefika kikomo... Ha ha ha nakwambia Doreen huna nafasi tena!"
Ilisikika sauti nyembamba na nyororo ikimwambia Doreen. Doreen alishtuka sana kusikia maneno Yale. Kilichomtisha zaidi ni kwamba alishindwa kumuona mtu aliyezungumza. "Kama una uwezo njoo nikuone!" Alisema Doreen. "Ha ha ha! Nitakuja unione wala usiwaze" maneno Yale yalizidi kumchanganya Doreen alibaki kimya akiwa ametumbua mimacho kama vitunguu huku akitazama huku na kule ndani ya chumba lakini bado hakufanikiwa kumuona mtu yule aliyezungumza kwa dharau sana.
"Naongea na huyu binti nilimfananisha na Dorice" alisema mama Dorice na kuwafanya majirani zake wageuke kumtazama Kwa mshangao. Hakujua watu wale wanashangaa nini lakini kilichowashangaza ni kwamba walimsikia mama Dorice akizungumza lakini hawakujua anaongea na nani kwani hawakumuona yule mtu. "Dada upo sawa?" "Nipo sawa ndio! Kwani vipi?" "Muda mrefu sana unaongea peke yako hapa..." "We Majaliwa tuheshimiane....
Nitaongeaje peke yangu kwani Mimi mwehu?" Alisema Mama Dorice kwa ukali kiasi. Abiria ndani ya gari ile walimshangaa sana mama Doreen wakahisi labda hayupo sawa kiakili kwani jirani yake kwenye siti hakuwa mwanamke Bali ni mwanaume mtu mzima mwenye umri kama miaka arobaini na tano.
Na kwa muda wote aliokuwa akizungumza Mama Dorice mwanaume yule alilala usingizi. "Dada hebu mtazame jirani yako vizuri" alisema Majaliwa. Mama Doreen alitamtazama jirani yake kwa makini sana. Ghafla akapatwa na mshtuko wa ghafla Baada ya kuona aliyedhani ni binti anayeendana sana na mwanaye si mwenye siti ile.
Aliyekaa pale ni mtu mwingine tofauti. Mama Dorice alishtuka sana, moyo ukampasuka paah! Hakuamini macho yake. "Kaka Majaliwa!" "Naam dada!" "Mbona sielewi Mimi? Ni mtihani gani huu?" "Labda una malaria dada?" "Sina chochote ila nilikuwa nimekaa na binti Fulani hapa. ." "Mmh! Hapo pagumu.." Mama Dorice alishindwa kuelewa chanzo cha yote hayo ikabidi akae kimya tu.
Macho yake yakatua dirishani na kutulia kwa muda kama aliyetazama kitu kilichomvutia sana. Ghafla akamwona Dorice dirishani( dirisha la gari) akimpungia mkono wa kumuaga kisha akaachia busu la mbali la upendo. Mama Dorice alishtuka sana akabaki ameduwaa tu mpaka Dorice alipopotea ghafla. "Kaka!" Aliita......
ITAENDELEA.....