RIWAYA YA MWANAFUNZI MCHAWI SEHEMU YA 36 na 37

RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 36 & 37
MTUNZI:ENEA FAIDY
...Mama Eddy alitazama juu ili kuona kama kuna chochote lakini hakuona kitu. Ilimbidi atumie nguvu zake za uchawi alizokuwa Nazo ili kujilinda kwani aliziona dalili za kuvamiwa katika mazingira ya kutatanisha.
Mama Eddy ambaye jina lake halisi alijulikana kama Maimuna hakuwa Mtu wa kawaida Bali alitumwa na uongozi mkuu wa himaya aliyotokea Doreen ili kumsaidia kupata vitu alivyovihitaji.
Alitumia mbinu ya kujifanya mke wa Mr Aloyce ili kuweza kumteka vizuri na kumfanya asihangaike sana kuhusu mwanae kwani kulikuwa na uwezekano mkubwa sana wa kuharibu kazi. Maimuna alikuwa ni kijakazi mkongwe wa Bi Tatile na alikuwa akiaminika sana katika himaya ya Wanatatile kwani ni mtu pekee aliyewahi kufanikisha ajali kubwa ya mabasi mawili iliyoua abiria wote kisha wakafanywa kitoweo katika sikukuu ya kumpongeza Bi Tatile kama kiongozi bora wa wachawi wote Afrika Mashariki. Bi Maimuna alikuwa akiaminika sana kwa kila kazi anayoagizwa kwani hakuwahi kufanya makosa zaidi ya tukio moja tu la kuanguka kanisani akiwa katika harakati za kuwanga mchana.
"Maimuna! Maimuna! Hapa sio kwako na Leo ndio mwisho wa ubaya wako kwenye familia hii" ilisikika sauti nyororo isiyo na mkwaruzo hata kidogo huku ikijirudia rudia. Maimuna alibaki na mshangao wa ajabu sana, akataharuki huku akihema kwa nguvu. Akaaangaza macho kila upande pasipo kumuona mtu yeyote.
Akazidi kuchanganyikiwa sana. Ghafla wazo likamjia akilini mwake, bila kuchelewa akaamua kulifanyia kazi. Akanyoosha mkono wake wake wa kulia kisha nguvu nyingi zikamjia kama radi mkononi mwake. Bi Maimuna akaachia tabasamu mwanana akiamini hakuna kitakachomdhuru kwa wakati ule wala wakati mwingine wowote. akatulia kimya akimsubiri adui yake, lakini hakuona chochote zaidi ya ukimya mzito uliokuwa umetawala.
"Kumbe unaniogopa eeeh!" Alisema Maimuna.
"Ha ha ha! Sikuogopi Maimuna... Nakuvutia pumzi tu maana sina papara" sauti ile iliyojaa dharau ilisikika. Bi Maimuna hakutushika hata kidogo kwani alikuwa anajiamini kupita kiasi. Ghafla sura yake ikabadilika sana na kuwa sura ya kutisha sana.
Meno yakawa marefu kama mnyama mkali, kucha zikawa ndefu na Kali kama za chui anayemvamia swala, macho yake yakawa meusi huku mboni yake ikiwa nyekundu kama moto. Lengo lake lilikuwa ni kuonesha nguvu zake mbele ya adui yake ambaye hakujua ni nani. Ghafla kicheko kikali cha kutisha kilichojaa dhauri na jeuri kikasikika na kumfanya Maimuna ajione mdogo kama simimizi ilihali hamjui nana aliyemcheka.
Wakati huo huo Mlango ulifunguliwa na Mr Aloyce aliingia sebuleni pale.
"Mamaaaa" Mr Aloyce alipiga ukunga wa nguvu baada ya kumkuta mkewe akiwa na umbile la kutisha sana. Uvumilivu ulimshinda alijikuta anakimbia nje kama chizi huku akihema kwa nguvu. Mlinzi alimshangaa Mr Aloyce bila kuelewa kinachoendelea.
"Vipi bosi?" Aliuliza mlinzi huku akicheka sana. Mr Aloyce alianguka chini kama mzigo huku akihema kama Mtu aliyepanda mlima mrefu kwa kasi. Mlinzi alimsogelea na kumuuliza kilichojiri.
"Kuna maajabu humo ndani"
"Maajabu gani?"
"Mke.. Mke wangu...Ame..."
"Amefanyaje tena?" Aliuliza mlinzi kwa woga kwani alishapewa onto Kali na mwanamke yule kuwa asimfatilie kwa lolote. Lakini kabla hajasema chochote kuna kitu kiliwashtua Mr Aloyce na mlinzi wakabaki wameduwaa kwa mshangao.
******
Mama Pamela hakuwa na la kufanya zaidi ya kulia tu. Muda wote ule hakujua Doreen anaendeleaje ila kilichomshangaza ni kwanini Doreen hakwenda sebuleni kujumuika nao? Alinyanyuka kitini na kwenda chumbani kwake. Lakini ghafla mshangao wa ghafla ulimvaa mwanamama yule baada ya kukuta hali ya chumba ni mbaya sana kila kitu kilikuwa shaghalabaghala tu, ndipo machale yakamcheza, akasogelea droo anayohifadhia pesa.
"Mungu wangu!" Alishtuka mama Pamela baada yakukuta droo IPO wazi lakini haina pesa yoyote zaidi ya stakabadhi ambazo hakuwa na shida nazo wakati ule. Macho yalimtoka kwa mshangao huku akitoatoa vitu ndani ya droo ile bila kuona chochote. Akasimama wima akiwa ameshika mkono kiunoni kwa hasira
"Doreen!" Aliita kwa jazba bila kujua Doreen alikwishaondoka muda mrefu uliopita. Mama Pamela akakugua tena ili kujiridisha kama kweli pesa hazikuwamo lakini bado hakukuta pesa ndani ya droo ile wala eneo lingine chumbani mle.
Mama Pamela alichanganyikiwa sana akatoka ndani ya chumba kile na kupiga hatua za harakaharaka koridoni kuelekea chumbani kwa Doreen.
Alifika mlangoni na kufungua mlango kwa jazba kubwa. Lakini cha ajabu chumba kilikuwa kitupu na hakukuwa na mtu yeyote wala dalili za uwepo wa mtu. Mama Pamela akahamaki, akamwita Doreen kwa sauti kali lakini hakuitikia.
"Mungu wangu ina maana Doreen ametoroka na pesa au?" Alijiuliza Mama Pamela akiwa ameishiwa nguvu kabisa. Hakutaka kuamini kama binti anayemuamini kiasi kile angetenda tukio lililotokea.
Mama Pamela alitoka nje ya nyumba yake ili kumtazama vizuri Doreen. Alimtafuta pale uani na kila upande wa nyumba lakini Doreen hakuwepo. Moyo wa mama Pamela ukatawaliwa na lawama nyingi sana. Akajilaumu ni kwanini hakumsikiliza mumewe mpaka yote hayo yametokea.
Akakaa chini kibarazani huku machozi yakimchuruzika. Kila akikumbuka maneno ya mwanae roho ilimuuma zaidi, hakuwa na hamu hata ya kula. Alikuwa na simanzi nzito iliyopelekea mafuriko ya machozi usoni mwake. Alilia mpaka machozi yakamkauka akiwa pale pale kibarazani kwake. Hakutaka hata kumwona binti yake kwani uchungu ungemzidia. Kwa jinsi alivyokuwa akimpenda na kumjali Pamela hakuamini kirahisi kuwa Leo amekuwa adui yake mkubwa na kumpa lawama za uchawi.
"Mungu tu Anajua" aliwaza Mama Pamela.
Majira ya saa kumi na moja jioni, Baba Pamela aliwasili jijini Mbeya na kufika nyumbani kwake akiwa na mawazo tele juu ya familia yake. Alipofika ndani tu alikutana na mkewe ambaye uso wake ulivimba sana kwa machozi ya siku nzima. Baba Pamela hakushangaa sana kwani alihisi mkewe anamlilia binti yao Pamela kumbe si hivyo tu, Bali alikuwa na jambo zito lililomtatiza sana moyoni mwake.
****
Familia ya akina Dorice ikiwa bado imekaa kikao babu yake Dorice aliyefahamika kama Mganga Tawi La Mtawile alikuwa tayari ametoa wazo kuwa atafanya jambo.
Familia nzima ikaondoka kwenye nyumba ya mama Dorice na kwenda moja kwa moja kwa Mganga Tawi la Mtawile ili kujua Dorice yupo wapi na katika hali gani.
Na kwakuwa hapakuwa mbali sana, walitumia mwendo wa dakika tano tu mpaka kufika kwenye nyumba ta Tawi La Mtawile.
Mganga yule maarufu mkoani singida, alikuwa ametenga eneo maalum nyumbani kwake kwaajili ya shughuli za uganga. Alipanga vyema vibuyu na dawa zake pembeni alizungushia kaniki nyeusi na nyekundu. Akavua viatu, kisha akawaamrisha wote waliombatana nae wavue viatu ndipo wakae kwenye zulia alilotandika chini. Wote wakafata kama walivyoamriwa.
Mganga Tawi alianza kuimba nyimbo za kuita mizimu na kuongea maneno ambayo wengine hawakuyaelewa . alitumia dakika kumi nzima kisha akachukua kioo kikubwa, akanyunyiza dawa na kuipakaza vizuri kwa kutumia mkia kama wa ng'ombe. Akaita jina la Dorice Mara tatu. Baada ya muda mfupi ardhi ikatetemeka sana radi zikapiga mfulululizo na kuwafanya wote waogope. Na kila mmoja alitamani kukimbia kwani palikuwa na utisho wa ajabu....
Riwaya:Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) -:Sehemu ya 37
....ukimya mzito ulitawala huku ndugu zake Dorice wakijiuliza ni mini kitatokea. Ghafla moshi mweusi ulioambatana na radi ukatokea mbele yao karibu na mti mdogo uliokuwa karibu na kile kijumba cha uganga cha Tawi La Mtawile. Wote wakakaza macho kwa woga huku wakitazama kwa makini moshi ule ulitokana na nini ilhali hakuna moto wowote katika eneo lile.
Kwa namna ya ajabu na ya kustaabisha sana ambayo hakuna aliyeitarajia. Doreen alitokea mbele yao akiwa na muonekano tofauti na waliomzoea. Alikuwa ni mrembo kupita kiasi huku marashi makali yenye harufu nzuri yakizidi kuziumiza pua zao kwa fujo, mikufu ya dhahabu ilining'nia shingoni mwake ikienda sambamba na hereni ilizokuwa amezivaa pamoja na Pete kwenye vidole vyake. Kila mmoja alionesha mshangao wa ajabu kwani hawakuelewa ni kwanini Dorice yupo vile. Walitulia kimya huku woga ukiwazidia kwani walijua ni mzimu wa Dorice.
"Dorice umekuwa jini?" Aliuliza Tawi la Mtawile kwa sauti Kali. Dorice akajiweka sawa na kuachia tabasamu mwanana huku akipiga hatua chache kuwasogelea ndugu zake ingawa hakuwa nao karibu sana.
"Kwanza kabisa nimefurahi kuwaona ndugu zangu... Mama nilionana nae tangu akiwa kwenye basi.." Alisema Dorice kwa sauti tulivu sana. Maneno yake yalimshtua sana Mama Dorice na kumfanya akumbuke matukio yote yaliyomtokea alipokuwa kwenye basi na kabla ya kuingia kwenye basi.
"Ni wewe?? Kwanini umekuwa jini?" Alisema Mama Dorice kwa sauti iliyojaa woga sana.
"Mimi sio jini ila ninataka kulipa kisasi na kuwakomboa watu wasio na hatia.." Alisema Dorice.
Baada ya Dorice kusema vile Wote wakatazamana kwa mshangao sana, mama Dorice alitaman mwanae Arudi katika hali ya kawaida ili aendelee kuishi nae lakini Dorice asingekubali hata kidogo kupoteza malengo yake aliyopangilia kuyafanya kwa wakati ule.
"Mama ninakupenda sana! Nina imani nitarudi nyimbani baada ya kumaliza kazi yangu... Asanteni kwa kuniita... Kwaherini!" Aliema Dorice kwa huzuni kubwa huku neno kwaheri likijirudia Mara kadhaa mpaka Alipopotea na kutoonekana tena machoni mwao. Huzuni ikamtanda mama Dorice akamtazama Mganga Tawi la Mtawile na kwa bahati wakagongana macho kwa mganga pia alikuwa akimtazama mama Dorice.
"Baba Naomba mwanangu arudi.." Alisema Mama Dorice huku chozi likimlengalenga machoni.
"Mmh! Hilo haliwezekani mwanangu... Dorice hakuwa duniani Bali aliolewa na jini na amepewa nguvu za kijini ambazo ni tishio sana... Ni kubwa kuliko kawaida na nadhani kuna jambo muhimu amekuja kulifanya maana lasivyo asingerudishwa duniani... Tawii..Tawi La Mtawileeee..!"
Alisema mganga yule kwa sauti Kali ya kiganga.
"Inamaana atakuwa jini?"
"Inawezekana akawa MTU wa ujinini siku zote"
"Eeh Mungu wangu" alisema Mama Dorice.
Mganga hakuwa na la kufanya juu ya Dorice. Wanaukoo wote walistaajabu lakini hawakuwa na la kufanya zaidi ya kupigwa na butwaa. Mama Dorice alikuwa haamini kilichomtokea mwanawe lakini hakuwa na jinsi na maneno ya mganga yalizidi kumpa mawazo mengi.
Haukupita muda sana wote walitawanyika na kwenda majumbani mwao huku suala la Dorice likiwa gumzo akilini mwao.
****
"Mama Pamela unakumbuka nilikuambia nini kuhusu mgeni wako?" Aliuliza Baba Pamela.
"Nakumbuka mume wangu" alijibu mama Pamela huku akilia. Na alijua fika kwa jinsi Baba Pamela alivyompenda mwanae basi lazima atafanya kitu kulingana na tuhuma zile alizoshtakiwa na mwanae.
"Umeona maisha mlioishi tangu amekuja?"
"Ndio.. "
"Vizuri...hebu muite hapa.."
"Hayupo... Nimemtafuta sijamwona..." Alisema Mama Pamela huku aibu na hofu vikizidi kumvamia kwa kasi sana kwani usemi usemao Asiye Sikia La Mkuu huvunjika guu ulitimia kwake kwa wakati ule ingawa hakuwa na imani kama Aliyemtoa titi binti yake alikuwa Doreen.
"Hayupo? Ameenda wapi?"
"Sijui...sijuii ameto...ametoroka... Na pesa amechukua!"
"Umeona sasa mke wangu? Umeona faida za ubishi e??"
"Nisamehe mume wangu..."
"Nilishakusamehe ila nilikuacha ujifunze.. Ila roho inaniuma sana kwa binti yangu.." Alisema Baba Pamela kwa huzuni. Maneno yake yaliibua tumaini jipya kwa mama Pamela na yakawa faraja tosha kwake. Lakini Pamela akawa kikwazo sana kwake kwani bado alikazania msimamo wake kuwa mama yake ndiye aliyemroga na kuchukua titi lake.
"Pamela mwanangu... Mama yako hawezi kufanya hivyo isipokuwa mwanazaya yule asiye na haya... Nilimwona tangu alipifika hapa ya kwamba ni mchawi ila mke wangu hakuelewa... Alimwamini sana binti yule mwenye sura ya kondoo kumbe chui"alisema Baba Pamela kwa sauti iliyojaa busara ya hali ya juu.
"Unamtetea mama.."
"Simtetei ila utaujua ukweli tu... Naamini Mungu wa Mbinguni atafanya muujiza wake hapa na lazima aliyekutenda hivi adhalilishwe.. In Jesus Name" alisema Baba Pamela mwanaume aliyekuwa anamcha Mungu kupita kiasi, alikuwa ni mwaminifu sana katika masuala ya Mungu kupita kiasi.
*****
Mr Aloyce na Mlinzi walistaajabu sana baada ta kumuona Mama Eddy (maimuna) akitoka nje mbio akiwa hajavaa nguo yoyote huku akihema kwa nguvu na kupiga mayowe hovyo.
"Nimekosaaa! Nimekosaaa" alilalama Mama Eddy huku akianguka chini na kujigaragaza kama mtu anayecharazwa viboko na nyaya za umeme.
Mr Aloyce na mlinzi walibaki wakiwa wamepigwa butwaa. Kila mmoja alishindwa la kufanya zaidi ya kumtazama tu mwanamke yule aliyeendelea kupiga kelele sana.
"Sirudiiii!sirudiiii nasema..." Alizidi kupiga kelele.
"Bosi kwani mama ana nini?" Aliuliza mlinzi.
"Unaniuliza nini na wewe si unamuona?" Alijibu Mr Aloyce.
Mama Eddy alihangaika kwa muda mrefu pale nje. Mr Aloyce aliingia ndani na kuchukua upande wa khanga ili akamsitiri mkewe lakini kila alipotaka kumfunika mkewe alikimbia kama chizi pale nje hakutaka hata kujifunika kwani alikuwa akiadhibiwa kupita kiasi bila kumuona MTU aliyemwadhibu. Mr Aloyce ilibidi atulie tuli na kumuacha mkewe aendelee kutaabika kwani yeye hakuwa na la kufanya.
Baada ya muda mrefu kupita. Mama Eddy akaanza kutulia kidogo huku akihema kwa nguvu lakini aliongea maneno ambayo hakuna aliyemwelewa.
"Mke wangu kulikoni?" Alisema Mr Aloyce kwa huruma.
"Nisamehe"
"Nikusamehe nini?"
"Nisamehe Mr Aloyce"
Mama Eddy aliendelea kuomba msamaga bila kutaja kosa lake alilolifanya. Na akiwa amekaa pale chini ghafla akaendelea kuisikia sauti iliyokuwa inamwongelesha tangu alipokuwa ndani.
"Na hapo bado... Mpaka mlipie mateso mliyowatesa watu wasio na hatia" "sirudii tafadhali" alisema mama Eddy huku akipiga magoti.
Mlinzi Na Mr Aloyce walishindwa kumuelewa Mama Eddy kwani walihisi anazungumza peke yake .
"Hurudii nini?" Aliuliza Mr Aloyce.
"Naomba nikwambie ukweli baba Eddy...mimi....!" Alisema Mama Eddy.
Wakati huo mlinzi yule alikuwa akiwaza vitisho alivyotishwa na mwanamke yule pindi alipofika nyumbani pale.
'Mh kumbeee ni mchawii' aliwaza mlinzi.
"Ukweli upi" aliuliza Mr Aloyce kwa mshangao kwani katu hakujua kama kuna kitu kinaendelea nyuma ya pazia...
Itaendelea...

Related Post

Previous
Next Post »