Waombaji wa Mikopo Elimu ya juu Wafikia 69,820 Mpaka Sasa

JUMLA ya wanafunzi 69,820 wameomba mikopo kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) hadi sasa
ikiwa zimebaki siku tatu kufikia mwisho wa kupokea maombi hayo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam , Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa bodi hiyo, Cosmas Mwaisoga, alisema mwaka jana walioomba kupewa mikopo walikuwa 65,000, hivyo waombaji wa mwaka huu wameongezeka.

Mwaisoga alisema tofauti na awali, mchakato wa sasa wa kuomba unafanyika kwa njia ya mtandao na baada ya kutumwa kwao, watayapitia na kwa yale yenye kasoro, wahusika wataitwa ili wayarekebishe.

Alisema dirisha la uombaji wa mikopo linatarajia kufungwa Jumapili hii.

Katika hatua nyingine, alisema idadi ya wanaorejesha mikopo imeongezeka maradufu baada ya kutakiwa kufanya hivyo.

“Kwa sasa ni vigumu kutaja idadi yao kwa sababu huwa tunaitoa mwishoni mwa mwezi kwa hiyo kesho tutakuwa na idadi kamili ya waliorejesha, lakini ikilinganishwa na huko nyuma, sasa hivi mwitiko wa wanaorejesha umeongezeka,” alisema.

Mwaisoga alisema sheria inamtaka aliyekopa aanze kurejesha baada ya mwaka mmoja wa kuhitimu masomo yake, lakini anapochelewesha, kila mwaka kunakuwa na penati ya ongezeko la asilimia sita.