RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 38 & 39
MTUNZI:Enea Faidy
.....Mr Aloyce bado hakumuelewa vizuri mkewe kwa kauli aliyoisema. Kauli ile iliibua utata mkubwa kichwani mwake na kumtaka mkewe amueleze ukweli.
"Niambie mke wangu... Nini kinaendelea? Maana Mimi sielewi!" Alisema Mr Aloyce kwa sauti ya upole ili mkewe amweleze ukweli wote. Lakini kwa bahati mbaya sana Maimuna alisita kueleza ukweli ambao alitaka kumwambia Mr Aloyce.
Viboko mfululizo vilivyosikika kwa sauti kubwa vilimshukia Maimuna na kumfanya ahangaike kupita kupita kiasi. Aligalagala pale chini kama nyoka aliyepondwapondwa kichwa chake. Sauti na yowe la kilio viliibuka kwa Maimuna kwani alishindwa kuvumilia maumivi ya viboko alivyochapwa na MTU asimfahamu.
"Nasemaaa!nasemaaa!" Alisema Maimuna huku akilia.
Mr Aloyce na Mlinzi wake walibaki na mshangao kwani kila walichokiona walihisi ni muujiza tu. Walibaki kimya huku wakimshangaa mwanamke yule.
"Aloyce... Mimi ni mchawiiii.." Alisikika Maimuna na kwa bahati mbaya sana alishindwa kuongea kwa sauti ndogo hivyo sauti ilipaa sana na kuwafanya wapita njia na majirani kujazana sana nje ya geti kwa Mr Aloyce. Kwa uzito wa adhabu alioipata Maimuna ilimbidi tu aseme ukweli wote uliomwacha mdomo wazi Mr Aloyce.
"Naitwa Maimuna.. Sio mama yake Eddy kama ulivyodhani..." Alisema Maimuna na kumfanya Aloyce ahamaki. Alichanganyikiwa sana na kushindwa kuzungumza.
"Nisamehe Aloyce... Nilikuja kuiteketeza familia yako.... Mkeo alishaliwa nyama ... Mimi nilikuja kumlinda Eddy ili sehemu zake za siri zibaki mikononi mwa Doreen"
"What? Ati nini? Kwanza Doreen ni nani?" Mr Aloyce alijikuta anauliza maswali matatu mfululizo huku hasira zikiwa zimempanda kupita kiasi. Alitamani achukue jiwe zito na kumponda nalo mwanamke yule.
"Ni mchawi... Alikuwa anasoma na Eddy..." Alisema Maimuna huku akilia kwa sauti kubwa.
"Oh! Shit!" Alisikika baba Eddy.
Watu waliokuwa pale nje walizidi kutafuta upenyo wa kuingia mle ndani. Lakini geti lilikuwa limefungwa, kelele nyingi kutoka nje zilizidi kusikika.
"Mchawiiiiii! Mchawiii! Tufungulie tumwadhibu huyo mchawiiii!! Funguaa! Mwanamke mchawi hafai kuishi!!" Sauti zile kutoka nje zilimhamasisha mlinzi kufungua geti na kuwaruhusu watu waingie. Cha ajabu watu wale waliingia wakiwa wameshikilia silaha za aina mbalimbali. Wengine mawe wengine visu huku wengine wakiwa wameshikilia fimbo na mapanga. Hali ilichafuka sana pale ndani.
Umati wa watu ulikuwa uvamia uwanja wa Mr Aloyce tayari kwa kumwadhibu mchawi aliyesababisha kilio na majonzi katika familia ya ile iliyokuwa imejaa upendo na amani hapo awali."Tuue tu... Afe Huyo" walisema. Ghafla Maimuna akabadilika na kuwa kiumbe tofauti na vile anavyofahamika wote wakashtuka.
*****
Doreen aliendelea kushangaa kwa hofu sana ndani ya chumba kile. Upepo mkali uliovuma chumbani mle na kuangusha baadhi ya vitu vilivyokuwa vimewekwa vizuri ulimfanya Doreen ajione mdogo kama sisimizi juu ya janga lile.
Akiwa bado haelewi la kufanya ghafla sura ya MTU aliyemfahamu ikatokea mbele yake na kumfanya Doreen apigwe na mshangao wa hali ya juu.
"Haa! Dorice!" Alisikika Doreen akiita kwa mshangao.
"Mimi hapa! Sema nikusikie!" Alisema Dorice kwa sauti iliyojaa dharau kupita kiasi. Kisha kabla hajaendelea na lolote akanyoosha kidole chake ukutani na ghafla kikatokea kama runinga pana iliyoonesha siku ambayo Doreen alimpaka kamasi usoni kiuchawi ili asipendwe na Eddy. Kisha akaonekana Doreen akimkata Eddy sehemu zake za siri.
"Ulikuwa mjanja sana sio?" Alisema Dorice. Doreen hakuamini macho yake alitetemeka kwa hofu kupita maelezo.
"Do..Dor...Dorice... Umepata wapi huo ujasiri wa kunitisha kiasi hicho?" Aliongea Doreen kwa kigugumizi sana. Dorice alimtazama Doreen na kucheka kidogo huku akitembeatembea ndani ya chumba kile.
"Ulininyang'anya penzi langu kinguvu kwa mtu nimpendae sana.. Cha ajabu ulitaka kumharibia yeye na familia yake... Kwanini wewe in katili na mbaya kitabia kuliko sura yako?" Aliuliza Dorice.
"Tafa..Tafadhali Dorice nisamehe.."
"Nimekusamehe tangu zamani... Ila nataka kukufunza adabu. Umeua wengi sana wasiokuwa na hatia umewaharibu wengi sana bila kosa." Alisema Dorice na kutoweka machoni mwa Doreen.
Doreen alichanganyikiwa mno, lakini kilia alipotaka kupotea na kumtoroka Dorice hakuwa na nguvu, kwani Dorice alikuwa na nguvu nyingi mno ambazo zilimsaidia kufanya kila alichokitaka. Na hakuna mchawi ambaye angeweza kumshinda Dorice kwa wakati ule.
Ghafla bin vuu! Kichapo kikali kikamshukia Doreen. Alihisi mawe mazito yanamshukia kichwani mwake na kumpiga kwa nguvu. Alihisi maumivu makali mno. Akapiga ukunga mkali baada ya kushindwa kuvumilia maumivu Yale. Hakuona sababu ya yeye kuendelea kukaa ndani ya chumba kile huku akitaabika akaamua kufungua mlango na kutoka nje ya chumba huku akilia kwa sauti kali . kilio chake kiliwashtua wengi na kuwafanya watoke njee kutazama kulikoni.
Umati wa watu ulifurika kumtazama Doreen pale nje. Alikuwa uchi wa mnyama huku akipiga kelele sana.
"Naacha uchawiii... Mimi si mchawi...uwiiiii... Nisaidieni" alilalama huku akipiga mbio bila kujali kuwa hajavaa nguo yoyote.
Watu walianza kumfuata huku wakipiga kelele "mchawii! Mchawiiii" "masikini we! Binti mzuri hivi kumbe ana mambo ya uchawi?" Walisikika watu wakiongea vikundi vikundi.
Watu walikazana kupiga picha huku wengine wakiokotw mawe na kumfukuza Doreen huku wakimtupia mawe.
Doreen alikimbia sana huku akipiga kelele sana.
Ghafla mama mmoja alipiga kelele sana
"Huyu mtoto aliinibia pesa zangu mgahawani kumbe ni mchawi! Alaaniwe!"
"Mimi alikuja dukani kwangu akataka aniwangie Leo ameumbuka" walizungumza yule mama wa mgahawa ambaye alitapeliwa na Doreen kwa mazingira ya kutatanisha sana ndipo alipojibiwa na mwanaume mwingine ambaye Doreen alijaribu kumuwangia ili aibe pesa.
Doreen alizidi kupiga mbio sana huku umati ule wa watu mjini Iringa ukizidi kumfata kwa kasi wakiwa wameshika mawe na wengine viboko.
*****
Baba Pamela alikuwa ametulia kidogo huku akimtazama binti yake kwa masikitiko makubwa.
"Daddy najisikia hasira hata kumtazama mama" alisema Pamela huku akilia.
"Hutakiwi kuwa hivyo... Nataka tufanye jambo hapa!"
"Jambo gani mume wangu?" Aliuliza mama Pamela.
"Nataka tumwombe Mungu mpaka atujibu juu ya binti yetu"
"Hakuna tatizo mume wangu.." Alisema mama Pamela kwani tayari maneno ya mumewe yalimpa nguvu hata ya kuzungumza.
"Pamela una amini kama Mungu anaweza kutenda mambo ambayo sisi hatuwezi?"
"Ndio naamini... Lakini..."alisema pamela
"Lakini nini? Ukiwa na imani hutakiwi kutilia shaka.."
"Sawa baba niombee tu.."
Baba Pamela aliwataka wote wapige magoti kisha wakaanza na nyimbo na baada ya hapo akaanza kufanya maombi. Aliomba sana akiwa anataka Mungu amrudushie mwanae titi lake.
Radi Kali zikaanza kupiga katika nyumba zilipiga radi nyingi wakati baba Pamela akiendelea kusali kwa bidii na imani sana. Ghafla akawaambia watoke nje wote.
"Roho wa Mungu ananiambia kuna kitu kimefukiwa pale nje ili kutuangamiza" alisema baba Pamela kisha wote wakatoka nje. Baba Pamela aliongoza njia mpaka Pale ambapo Mama Pamela alifukia sahani iliyokuwa na kinyesi. Wakafukua.
Cha ajabu akatokea nyoka mkubwa sana ambaye hakuna aliyetarijia kama angekuwa pale.
"Mungu wangu!" Alisikika Mama Pamela akizungumza kwa woga. Baba Pamela alizidi kumwomba Mungu mpaka yule nyoka alipobadilika na kuwa na sura ya Doreen lakini mkiani akabaki kuwa nyoka. Wote walistaajabu sana huku wakitetemeka kwa woga...
RIWAYA:MWANAFUNZI MCHAWI - SEHEMU YA 39
...."Ina maana Doreen ni mchawi kiasi hiki?" Alijikuta anaropoka kwa mshangao mama Pamela. Pamela alizidi kushangaa huku akimtazama mama yake kwa mshangao kisha akimtazama chatu yule mwenye sura ya Doreen. Baba Pamela aliendelea na maombezi yake kwa imani kali. Yule chatu alijigeuza geuza kwa vitisho vikali sana huku akijaribu kupambana Na Baba Pamela kwa kujitoa kwenye lile shimo dogo.
Lakini kwa bahati njema chatu yule alipigwa na radi Kali sana iliyoharibu uso wake na kuweka mipasukopasuko iliyoacha damu ichuruzike kirahisi. Baba Pamela hakuacha kuomba na kuithibitisha imani yake thabiti. Ghafla ukatoka moshi mkali kutoka kwenye mdomo wa sura ya Doreen iliyopo kwa yule chatu.
Moshi ule ulikuwa wa ajabu sana Kwani ulikuwa katika mstari ulionyooka mpaka kifuani kwa Pamela, na hata Pamela alipojaribu kukimbia moshi ule ulimfuata kila alipoenda na kumfanya Pamela aogope zaidi. Pamela alipoona hawezi kuukwepa moshi ule akasimama wima akisubiri kuona kitakachotokea huku akihema nguvu sana.
Moshi ule ulitua taratibu kifuani kwa Pamela kisha ule mstari uliokuwa umejitengeneza ukapotelea kifuani kwa Pamela taratibu sana. Pamela alijishangaa sana Kwani alihisi mabadiliko Fulani mwilini mwake. Alitulia kimya huku akimtazama baba yake.
Baba Pamela alipohitimisha maombi yake yule chatu alipigwa radi Kali kisha akatoweka machoni kwa wanafamilia wale.
"Jina la Bwana lihimidiwe kwani ametenda tulichokitaka.. Amejidhihirisha mbele yetu.. Oh asante Bwana wa Majeshi" alisikika baba Pamela huku akiinua macho yake na mikono yake juu ili kumshukuru Mungu kwa ajili ya maombi yake.
"Pamela hebu jitazame kifuani kwako" alisema Baba Pamela huku akitabasamu na kutoa kitambaa laini mfukoni na kujifuta jasho lililokuwa limetapakaa usoni kwake kama chemchem ya maji.
Mama Pamela alimsogelea mwanae na kumsaidia kushuhudia kilichotokea kifuani kwake. Walisogea pembeni kidogo, kisha Pamela akajifunua shati lake na kujitazama kwa umakini. Wote hawakuamini kilichotokea kwani titi lake lilikuwa limerudi kama lilivyokuwa. Pamela alishtuka sana na kupiga kelele za shangwe huku akiruka kama ndama. Akamkimbilia baba yake na kumkumbatia kwa nguvu.
"Baba! Nashukuru baba! Asante!" Alisema Pamela kwa furaha kuzidi kiasi.
"No Pamela! Mshukuru Mungu sio mimi" alisema Baba Pamela huku akitabasamu.
Pamela alimuachia baba yake na kumfuata mama yake, chozi likamdondoka kwa uchungu huku akimkumbatia mama yake.
"Nisamehe sana mama! Naomba unisamehe kwa kukufanya ukose amani na kujisikia vibaya kwaajili yangu. Nakupenda sana mama.. Nisamehe mama!" Alisema Pamela huku akilia kwa uchungu.
"Pamela mwanangu! Usijali kwa yote yaliyotokea nilishakusamehe" alisema mama Pamela huku akimkumbatia kwa mahaba mazito binti yake mpenzi.
Baba Pamela alisimama pembeni yao kisha akapiga hatua za taratibu na kuwasogelea.
"Mke wangu... Familia yetu ingekuwa pabaya sana kwaajili ya yule adui! Lakini ni funzo kwako kuwa usimwamini kila mtu pia jifunze kumcha Mungu kwa moyo wote"
"Ashukuriwe Mungu sana! Tangu Leo wote tutamcha Mungu" alisema Mama Pamela.
"Kweli kabisa.. Mungu ni mkuu" alisema Pamela kisha Wote wakakumbatiana kwa furaha, ile furaha ya mwanzo ikawa maradufu. Kila mmoja alionekana kufurahi sana ule umoja uliotaka kuvurugika ukarejea tena katika familia ile ikazidi kung'ara na kuwa familia bora.
"Hakuna wa kumfananisha na Mungu!" Walisema kwa pamoja huku wakiwa na furaha ya ajabu.
*****
Leyla alipokea ugeni kutoka kanisani kwake ambapo wanamaombi watano walitia timu nyumbani kwake na kuiikuta familia ile ikiwa imepoteza furaha kabisa.
Leyla aliwakaribisha wageni wake vizuri na kuwakaribisha viti.
Mwalimu John na Judith walikuwa wapo kimya tu ingawa moyoni mwao walifurahia ujio wa watu wale.
Leyla akaamua kuwaambia kila kitu kilichotokea ndipo Walipoanza maombi yao. Walijtahidi kusali kwa imani kubwa sana. Baada ya maombi ya kama SAA zima ndipo maombi yao yalipoanza kujibiwa. Mambo ya ajabu yalianza kutokea ambApo mwalimu John alianza kuzungumza lakini cha ajabu funza walianza kutoka tena miguuni.
"Kuna mtu ni mchawi hapa" alisema Mwalimu John na kuwafanya wote wastaajabu.
"Tulia mume wangu watu wanakusaidia..." Alisema Leyla akimwambia mumewe.
"Nasema kuna Mtu anaroga hapa... Atoke.." Maneno hayo ya Mwalimu John yaliwafanya wote watazamane na kusitisha maombi kwa muda. Mwalimu John aliendelea kuongea.
"Wewe acha kuroga maombi ya wenzako... Wewe! Nikuseme?" Alisikika mwalimu John wakati huo wote walikuwa wameinamisha sura zao chini wakiogopa kutajwa. Baada ya dakika kadhaa kupita Mwalimu John alimsogelea mwanamke mmoja na kumshika bega.
"Sema ukweli la sivyo hawa funza wanahamia mwilini mwako.." Alisema mwalimu John huku akimkazia macho mwanamke yule.
"Mi..mimi..nime.. Mimi.." Alibabaika yule mwanamke.
"Ukidanganya tu funza wanakuhamia..."
"Ahm..aah.. Kweli.. Nilitaka..nilikuwa naroga msiendelee na maombi.." Alisema yule mwanamke akiwa anaona aibu kupita kiasi.
"Haya tokaa" aliamrisha mwalimu John na yule mwanamke akaondoka haraka huku kila mtu akimtazama kwa mshangao.
Hawakupoteza muda maombi yakaendelea na hawakutumia muda mrefu sana funza kwa mwalimu John wakapotea wote. Na mara ile Judith aliona ulimi wake ukiwa mwepesi sana na akaweza kuongea. Mwalimu John alikuwa kama aliyetoka usingizini alishtuka mno kuona kila kinachoendelea.
"Jamani.. Doreen ulitaka kuniua? Kwanini Doreen?" Alisema mwalimu John.
"Doreen ni nani?" Aliuliza mwanamaombi mmoja.
"Ni mwanafunzi wangu... Ni mchawi sana alitaka kuniua na alinifanyia mambo ya aibu sana" mwalimu John akasimulia kila kitu kuhusu Doreen.
Judithi pia akaeleza kila kitu kilichompata Mwalimu Jason ambaye tayari alishafariki dunia.
"Oh poleni sana watumishi Mungu ni mwema... Cha msingi mumrudie yeye!"
"Amen!"
Hatimaye mwalimu John na Judith wakarudia hali ya kawaida na furaha yao ikarejea tena. Walimshukuru sana Mungu.
Mwalimu John alimsogelea mkewe na kumbatia kwa dhati na upendo.
"Asante kwa upendo wako wa dhati uliokufanya uwe mvumilivu mno kwangu... Nakupenda!" Alisema mwalimu John na Leyla akatabasamu tu.
Wanamaombi wale walishukuru Mungu na kuwasihi familia ile pamoja na Judith kutomuacha Mungu. Kisha wakaondoka zao.
*****
Doreen alipokuwa anakimbia ndivyo kadri kipigo kilipomzidia. Kwani aliadhibiwa sana na Dorice na wakati huohuo Mungu alikmwadhibu kupitia maombi ya watumishi wake waaminifu.
Doreen alihisi mwisho wake umefika. Alilia kwa uchungu huku akipiga hatua za kichovu kuelekea nyumbani kwa kina Eddy kama Alivyoambiwa na Dorice ili akajisalimishe na kuombs msamaha.
Safari ilikuwa ndefu kwa binti yule aliyeuwa watu wengi shuleni kwao na kuwadhuru walimu wake wasiokuwa na hatia.
Hakuwahi kufika nyumbani kwa akina Eddy lakini alifika bila kupenda.
Umati wa watu uliokuwa nyumbani kwa mr Aloyce uliongezeka zaidi baada ya Doreen kufika pale.
Kulizuka hali ya tafrani katika eneo lile.
"Mimi ndo Maimuna halisi... Sio mama Eddy kama ulivyodhani.." Alisema Maimuna akiwa na sura mbaya kupita kiasi. Alikuwa ni mweusi mithili ya mkaa wa chunya, macho makubwa makali, mekundu kama pilipili, alikuwa na tumbo kubwa sana lililojaa michiriz, nywee zilikuwa chafu tena zimesokotana sana huku midomo yake mipana myeusi ikiyasitiri meno yake yaliyokaa hovyohovyo kinyani mwake.
Mr Aloyce aliishiwa nguvu, alishindwa kulia akadhindwa kuongea akabaki kimya amejiinamia.
Ujio wa Doreen na umati mwingine wa watu ukawa utata mwingine kwa Mr Aloyce.
"Nisamehe Eddy..." Alisikika Doreen akilia kwa sauti na wakati huo Eddy alikuwa anatembea taratibu kutokea ndani na kuja kymushuhudia kinachoendelea. Waandishi wa habari walikuwa wengi wakipiga picha tukio lile la ajabu.
Itaendelea....