RIWAYA YA MWANAFUNZI MCHAWI SEHEMU YA KUMI NA NANE

RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya Kumi na Nane
MTUNZI : ENEA FAIDY
...MAMA Eddy aliendelea kukoroma kwa nguvu pale chini na kuzidi kumchanganya sana mumewe Mr.Alloyce. Mwanaume yule alichanganyikiwa haswa na kujikuta akiangusha chozi lake kwa uchungu kwani alishindwa kuielewa hali ya mkewe. Alimuita Mara kadhaa lakini Mama Eddy aliendelea kukoroma tu bila kujibu neno.
Mr.Alloyce akazidi kuchanganyikiwa sana bila kuelewa afanye nini na kwa wakati ule hakukuwa na msaada wowote katika eneo lile. Akachukua simu yake na kuitafuta namba ya rafiki yake haraka kisha akapiga lakini alipopiga tu akakutana na maandishi haya " Emergency call only" ndipo akagundua kuwa sehemu aliyokuwapo haikuwa na mtandao, akazidi kuogopa huku huzuni ya kupotelewa na mkewe ikimvaa kwa kasi ya ajabu. Kwa muda wote huo hakuna gari yoyote ilipita eneo lile.
"Na..na..nakufa..nakufa mume ..wangu.." Ilisikika sauti ya mama Eddy.Sauti ile ya mama Eddy ilikuwa kama mwiba mchongoma uliopenya katikati ya moyo wa Baba Eddy. Hakuamini kile alichokisikia kwa mkewe akahisi ilikuwa ndoto tu isiyokuwa na ukweli wowote.
"Usife mke wangu.. Usife mpenzi wangu!" Aliropoka Mr.Alloyce lakini tayari alikuwa amechelewa sana kwani mkewe alikuwa tayari amekata roho.
"Mke wangu! Mke wangu!" Baba Eddy alijaribu kumuita mkewe lakini tayari alikuwa ameaga dunia. Simanzi ilimjaa Mr. Alloyce alijkuta Analia kama mtoto mdogo huku akijigaragaza chini kama mwendawazimu. Alilia kwa uchungu sana kwani alimpenda mkewe kwa dhati na hakuwa tayari kumpoteza. Alikuwa ndiye ndugu yake pekee aliyesalia kwani Mr.Alloyce hakuwa na kaka, Dada wala wazazi.
Wakati akiwa ameushikilia mwili wa mkewe ghafla akajikuta hajashika chochote mkononi mwake zaidi ya gauni alilokuwa amevaa mkewe, ndilo pekee lililombakia mkononi. Akashtuka sana, akajaribu kupepesapepesa macho huku na kule ili aone mkewe ameenda wapi lakini hakumuona. Mr. Alloyce akainuka pale chini haraka na kuanza kutimua mbio kwani alishaona hali si shwari.
Alikimbia kwa muda mrefu bila kujijua anakimbiaje mpaka pale fahamu zake halisi zilipomrudia ndipo akasimama kidogo na kupumzika. Alihema kwa nguvu huku akiwa amejibwaga chini ghafla akasikia mlio mkali ukimjia nyuma yake. Mr.Alloyce akainuka chini na kuanza kukimbia tena lakini akiwa katika mbio hizo akapata ufahamu tens akasikiliza tena ule mlio akagundua ni mlio wa honi ya gari.
Akaamua kusimama ili aombe msaada. Baada ya muda ya sekunde kadhaa basis la abiria likitokea Dar es salaam lilikaribia mahali alipo Mr.Alloyce ndipo alipoanza kupunga mkono ili aombe msaada.
Dereva wa basi lile alikuwa mwelewa sana, akasimamisha gari na kumsaidia Mr. Alloyce aliyekuwa akihema sana. Mr.Alloyce alishukuru sana akaingia ndani ya basi.
"Vipi mbona umeshika gauni hilo mkononi?" Aliuliza kondakta baada ya kumkagua kwa macho Mr.Alloyce
"We acha tu.." Alijibu Mr. Alloyce huku akihema sana.
"Isije ikawa umeua huko halafu sisi tumekusaidia hapa...!" Alisema kondakta.
Mr. Alloyce alikataa kwa kichwa tu kwani hakuweza hata kujibu kutokana na maswahibu yaliyomkuta.
"Haya.. Unashuka wapi?"
"Naenda Ipogoro Iringa!" Alisema Alloyce na kuinamisha kichwa huku akilia.
******
Doreen alishindwa la kufanya mbele ya mwalimu wake pamoja na Matron alibaki ameduwaa tu lakini cha ajabu hakuonesha aibu yoyote. Alijikausha kimya tu akiwatazama.Mwalimu Amina na Matron walomsogelea Doreen kwa woga.
"Unaumwa nini?" Aliuliza Matron
"Kichwa!"
"Pole! Nakuletea dawa!" Alisema matron kwa sauti ya upole sana.
"Asante" alijibu Doree kwa sauti ya chini kidogo ila kwa kujiamini sana.
Matron na Madam Amina walitoka. Doreen aliinuka pale chini na kuvaa nguo zake kisha akajifuta madawa yake usoni.
"Huku ni kudhalilika sana ingawa nimejikaza kisabuni, duh!" Aliwaza Doreen huku akirudisha vitu kwenye sanduku lake.
Matron na madame walibaki na maswali mengi sana vichwani mwao. Kila mmoja alijiuliza kivyake lakini uvumilivu ukawashinda. Wakajikuta wameanza kuulizana ili wasaidiane kupata majibu wakati huo wakielekea kwenye dispensari ya shule kuchukua dawa.
"Hivi we umemuelewa yule mtoto?" Aliuliza matron kwa sauti ya chini.
"Mh! Nikajua we umemwelewa.. Sijamwelewa! Lakini nimepata jibu la kitu kimoja..." Alisema madam Amina huku akipunguza sauti na kumsogelea vizuri matron.
"Nini tena?"
"Nilisikia kuwa huyu binti ni mchawi na ndiye aliyesababisha majanga yote haya hapa shule na niliongea na afisa elimu kuhusu hilo.."
"Mh! Afisa elimu hataelewa maana kama ujuavyo serikali haiamini uchawi!"Alisema matron.
"Nilizongea nae kiutu tu.. Na Leo nimpata picha ya huyu mtoto kwenye simu..!"alisema madam Amina huku akifungua picha kwenye simu na kumuonesha Matron. Ilikuwa ni picha iliyomwonesha Doreen jinsi alivokuwa kule chumbani. Matron alishtuka kidogo kwa ujasiri aliokuwa nao madam Amina mpaka akampiga picha Doreen.
"Nimeamua nimpige hii picha kama uthibitisho... Nimempiga kwa uangalifu sana ... " alisema madam Amina huku akimpigia simu Afisa elimu ili afike shuleni pale na waweze kumfukuza shule Doreen kama walivyokubaliana na Afisa Elimu.
"Sasa mna vithibitisho?"
"Hapa hakuna kutumia serikali la sivyo tutaisha... Huyu afisa elimu tumeongea mengi ambayo huwezi kuelewa..!"
Alisema Madam Amina kwa kujiamini sana kisha matron akachukua dawa za kutuliza maumivu na kuelekea bwenini kwa Doreen. Njiani alikuwa akimpigia simu Afisa elimu lakini hakupatikana.
Walifika bwenini ili wamkabidhi Doreen dawa. Lakini walichokikuta wakabaki wanatazama kwa mshangao wa hali ya juu.
*****
Mwalimu Jason alitamani amzuie mpenzi wake Judith asilale kitandani kwake lakini hakuweza. Judith alikuwa tayari amejilaza kitandani kwa Jason.
"Judith ndo tabia gani?"
"Ipi? "
"Umefika hata hajaongea chochote unalala? Kwanini?"
"Kama huna muda na Mimi nifanyaje?"
"Uvofanya sio bhana! Inuka basi njoo sebuleni.."
"Sitaki!"
Sijui ni shetani gani aliyempitia Judith siku ile maana alikuwa king'ang'anizi wa mambo kuliko kawaida. Licha ya mwalimu Jason kumkatalia kulala kitandani pale lakini Judith hakumwelewa hata kidogo.
Mwalimu Jason alibaki kimya huku malumbanoakali yakiendelea kichwani mwake. Alikuwa haelewi aamue nini kati ya kifo chake au kukata titi la Judith. Alikuwa na mapenzi ya dhati sana kwa mwanamke yule lakini Leo hii shetani alitaka aingilie kati kuvuruga penzi lao. Mwalimu Jason alikaa chini machozi yakimbubujika. Judith aligundua kuwa mpenzi wake alikuwa Analia moyo wake ukashtuka kwani daima hakupenda kuona mpenzi wake akiwa katika halo ya huzuni.
Akainuka kitandani na kumfuata Jason pale alipokuwa ameketi.
"Baby! Mbona unalia?" Aliuliza Judith kwa sauti ya mahaba yenye kubembeleza. Lakini Jason hakujibu kitu zaidi ya kuendelea kulia.
"Nisamehr mpenzi nilikuwa nakutania tu.. Kwani hujazoea utani wangu baby?" Masikini Judith alianza kujitetea akidhani amemkosea mpenzi wake bila kujua kuwa uhai wake ulikuwa hatarini sana. Jason hakujibu kitu, akaendelea kulia tu na kumfanya Judith ajisikie vibaya sana na kuhisi kuwa alimkosea mno Jason. Judith akaendelea kuomba msamaha lakini ilikuwa kazi bure.
"Hujanikosea!" Jason aliamua kimjibu Judith. Na wakati huo kuna sauti aliyoisikia masikioni mwake ikimwambia"Chukua titi haraka!" Jason akaongeza kilio.
Sauti ile ilizidi kumsisitiza mpaka akajikuta anainuka na kutoka chumbani mle. Judith alibaki kajiinamia akijiuliza mini kimemkumba mpenzi wake. Ghafla akainua kichwa ns kumuons Jason akimjia huku ameshika kisu kikali sana.
"Vipi baby?" Aliuliza Judith kwa mshangao.
"Nakupenda sana.. Ila...inanilazimu!' Alisema mwalimu Jason huku akimsogelea Judith. Judith alitoa macho kwa hofu..
Itaendelea.......